TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) mkoani Mara, inamshikilia Mkurugenzi wa Kituo cha Makoye
Education Centre kilichopo Nyasho Manispaa ya Musoma, Mwalimu Joseph
Makoye, kwa tuhuma za kudai rushwa ya ngono.
Inadaiwa alidai rushwa ya ngono kwa
mwanafunzi aliyekuwa akifanya maandalizi ya kufanya mtihani wa taifa wa
kidato cha nne kwa mwaka 2013 kituoni hapo unaoanza leo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari na Mkuu wa Takukuru mkoani Mara, Holle Makungu, ilidai mwanafunzi
huyo ambaye jina lake linahifadhiwa, alijiandikisha kufanya mtihani huo
kupitia sanduku la posta 216 la kituo hicho, ambapo barua yake ya
mtihani kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NACTE) ilipitia katika kituo
hicho na ndipo mkurugenzi wa kituo hicho alipotaka apewe rushwa ya
ngono aitoe barua hiyo.
Taarifa hiyo ilidai baada ya barua hiyo
kupokelewa katika kituo hicho, ilishikiliwa na mtuhumiwa ambaye kimsingi
ndiye mmiliki wa sanduku hilo la barua kwa jina la Makoye Education
Centre na kushindwa kumpa binti huyo hadi apewe rushwa ya ngono ikiwa ni
sharti la kuipata barua hiyo.
Taarifa hiyo ilidai kuwa mtuhumiwa
alitoa tahadhari ya kama binti huyo hatatoa rushwa hatoweza kufanya
mtihani wake, kwa kuwa asingempatia barua hiyo.
Kutokana na hali hiyo, binti huyo
alikwenda kutoa taarifa Takukuru ambapo iliandaa mtego wa kumnasa
mtuhumiwa huyo katika eneo hilo Oktoba 2, mwaka huu, saa moja usiku
baada ya mtuhumiwa kumpigia simu mwanafunzi huyo na kumtaka aende hapo.
Alisema maofisa wa Takukuru wakiwa
katika mtego wao, alifika mtuhumiwa katika eneo hilo kisha kumuita
mwanafunzi na kumpandisha katika gari lenye namba za usajili T 697 BNQ
kisha kwenda naye katika nyumba ya kulala wageni ya Tedasi iliyopo eneo
la Bweri nje kidogo ya Mji wa Musoma.
Alisema walifanikiwa kumtia mbaroni
mtuhumiwa huyo katika nyumba hiyo ya wageni kisha kwenda naye nyumbani
kwake eneo la Mkendo Kati na kufanya upekuzi na kufanikiwa kuipata fomu
hiyo kutoka NACTE.
“Uchunguzi zaidi wa tukio hilo bado
unaendelea na utakapokamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa
dhidi ya mtuhumiwa huyo,” alisema Makungu.
No comments:
Post a Comment